Hukumu ya uchaguzi wa Kenya yasubiriwa

Mahakama ya juu kabisa ya Kenya leo itatoa uamuzi juu ya kesi ambayo inapinga ushindi wa Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa awali mwezi March.

Mawakili wa mpinzani wa Bwana Kenyatta, Raila Odinga walimaliza kutoa hoja zao ambapo kila upande ukisisitiza kuwa una ushahidi wa kutosha.

Lakini sasa wanasubiriwa majaji sita ambao wamekuwa wakisikiliza kesi hiyo kutoa uamuzi wao.

Raila Odinga alikwenda mahakamani akidai kuwa uchaguzi uliofanywa tarehe 4 March ulikumbwa na dosari nyingi na huenda Bwana Kenyatta hakutimiza kipengee cha katiba, ambacho kinamtaka rais awe amepata zaidi ya asili-mia-hamsini ya kura.

Uamuzi wa mahakama hiyo ya juu ya Kenya ni ya mwisho, na kulingana na katiba ya nchi, hauwezi kubatilishwa.