Jeshi lauwa wapiganaji 14 Kano

Wakaazi wa Kano, Nigeria

Wanajeshi wa Nigeria wanasema kuwa wamewauwa watu 14 wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Boko Haram katika shambulio dhidi ya jengo moja mjini Kano, kaskazini mwa nchi.

Msemaji wa jeshi alieleza kuwa mwanajeshi mmoja alikufa katika shambulio hilo, na mshukiwa mmoja alikamatwa kwenye gari lilojaa mabomu.

Ulinzi umezidishwa kukiwa na wasi-wasi kuhusu usalama wa Wakristo wakati wa Pasaka.

Jeshi la Nigeria linasema wanajeshi walishambulia nyumba iliyoaminiwa kuficha wapiganaji wa Kiislamu, baada ya gari kuvuka kizuizi cha jeshi.

Limesema kuwa wanajeshi walikuta silaha na gari lilosheheni mabomu ndani ya uwa wa nyumba hiyo, ambayo iliangamizwa.

Inasemekana shahidi mmoja alimuona mwanamke na mtoto kati ya waliokufa.

Jeshi mara nyingi linapunguza hasara inayopata na linawajumuisha wote waliouwawa kuwa wapiganaji.

Makundi ya kutetea haki za kibinaadamu yanasema wanajeshi mara nyingi wanauwa raia katika operesheni zake dhidi ya wapiganaji.