Kiongozi wa waasi 'CAR' ajitangaza Rais

Image caption Kiongozi wa waasi katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati,Michel Djotodia

Kiongozi wa waasi katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, amejitangaza kuwa rais wa nchi na hata kutangaza serikali ya mpito ambako anasimamia wizara kadhaa.

Michel Djotodia, anayesema kuwa ataongoza nchi hadi uchaguzi utakapofanyika mwaka 2016, aliamkuliwa na mamia ya wafuasi wake mjini Bangui, siku ya Jumapili.

Wiki moja iliyopita, alimng'oa mamlakani rais Francois Bozize, aliyekimbilia kwingineko.

Wapiganaji wa waasi walivamia mji wa Bangui baada ya mkataba wa amani kutupiliwa mbali.

Rais aliyeng'olewa mamlakani, mara ya kwanza alikwenda Cameroon, kabla ya kuomba hifadhi nchini Benin.

Muundo wa serikali ya mpito ulitangazwa moja kwa moja kupitia redio ya taifa.

Nicolas Tiangaye, kiongozi wa upinzani aliyefanywa kuwa waziri mkuu baada ya makubaliano ya kugawana mamlaka, alisalia katika wadhifa wake.

Wanachama wengine wanane wa uliokuwa upinzani pia watafanywa mawaziri katika baraza la mawaziri 34.

Bwana Djotodia, aliyejitangaza kama rais, atakuwa waziri wa ulinzi, wakati wanachama kadhaa wa kikundi cha waasi wa Seleka, watasimamia wizara zengine.