Mandela hospitalini kwa siku ya sita

Image caption Maombi yaliyofanywa kwa niaba ya Mandela na raia wa Afrika Kusini

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, yuko hospitalini kwa siku ya sita ambako anatibiwa homa ya mapafu.

Madaktari wanasema kuwa amapeta nafuu.

Kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili jioni, Mandela mwenye umri wa miaka 94, aliweza kupumzika vyema na kuwa angali anapokea matibabu.

Mandela amelazwa hospitali hii ikiwa mara ya nne katika kipindi cha miaka miwili.

Hata hivyo hakuna taarifa zozote zimetolewa kuhusu muda atakaokuwa hospitalini.

Bwana Mandela aliugua kifua kikuu kwa mara ya kwanza mapema miaka ya themanini wakati alipokuwa amefungwa jela katika kisiwa chaRobben.

Mapafu yake yanasemekana kuathirika wakati huo alipokuwa anafanya kazi katika machimbo ya mawe.

Mwishoni mwa wiki, makanisa kote nchini humo walifanya maombi kwa niaba ya Mandela, aliyepigania uhuru dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Rais Jacob Zuma, aliwashukuru maelfu ya waafrika Kusini waliomuombea Madiba katika makanisa mbali mbali.