Korea Kaskazini kufungua vinu vya nuklia

Image caption Picha ya Satelite ya mtambo wa nuklia wa Korea Kaskazini mjini Yongbyon

Korea Kaskazini inasema itajenga upya na kufungua vinu vyake vya nuklia.

Hii ni pamoja na kituo cha kuimarisha madini ya uranium na kinu katika eneo la Yongbyon, kilichofungwa baada ya makubaliano ya kimataifa mwaka 2007.

Wakuu wanasema uamuzi huo utaimarisha uwezo wa kinuklia wa Korea Kaskazini na kuisaidia kukabiliana na upungufu mkubwa wa nguvu za umeme.

Katika siku za hivi punde, Korea kaskazini imetoa matamshi makali kufuatia mazoezi ya kijeshi yanayoendelea na ambayo yanayoshirikisha vikosi vya Marekani nchini Korea Kusini.

Hatua hii ni ya hivi karibuni na ni miongoni mwa hatua za Pyongyang tangu kufanya jaribio la tatu la nuklia mwezi Februari.

Imeghadhabishwa na hatua za kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa pamoja na mazoezi ya pamoja ya jeshi la Marekani na Korea Kusini

Katika wiki za hivi karibuni, taifa hilo la kikomunisti, limetoa onyo kadhaa dhidi ya Korea Kusini na Marekani onyo ambalo limesababisha Marekani kuchukua hatua kadhaa mfano kuhamisha ndege na zana zingine za kijeshi kuzunguka rasi ya Korea.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini , amesema kuwa ikiwa ni kweli, hatua ya Korea Kaskazini itakuwa jambo la kusikitisha sana.

Mtambo wa Yongbyon ambao umekuwa chanzo cha madini ya plutonium yaliyotumika kwenye silaha za nuklia za Korea Kaskazini, ulifungwa Julai mwaka 2007 kama sehemu ya mpango wa kupewa msaada huku ikitakiwa kusitisha shughuli za kuuza zana za kivita.

Moja ya sababu ya mkataba kusambaratika, ilikuwa kwamba Marekani haikuamini kuwa ilisalimisha silaha zake zote, jambo lililotiliwa shaka na hata kuthibitishwa wakati Korea Kaskazini ilipomruhusu mwanasayansi wa Marekani Siegfried Hecker kuona kinu chake cha madini ya Uranium eneo la Yongbyon mwaka 2010.