Mkataba wa kudhibiti silaha wapitishwa

Mkutano mkuu wa Umoja wa mataifa umeidhinisha kwa kiasi kikubwa mkataba wa kwanza wa kimataifa unaohusu udhibiti wa biashara ya mabilioni ya dola ya silaha.

Nchi 154 zimeunga mkono mkataba huo, 3 zikaupinga huku 23 zikisusia kupiga kura.

Sasa azimio hilo limeweka sheria kali zitakazo simamia uuzaji nje wa silaha za aina yote.

Nchi zote zitalazimika kuripoti mauzo yote ya silaha na kufanyia uchunguzi mwanzao iwapo kuna hatari yoyote ya silaha hizo kuishia kutumiwa kudhalilisha haki za binadamu.

Iran, Syria na Korea ya kaskazini ndizo zilizopinga azimio hilo.

Waliounga mkono wanasema kuwa hii ni hatua kubwa baada ya zaidi ya miaka kumi ya kupigania udhibiti huo.

Hata hivyo baadhi ya wadadisi wanahoji iwapo hatua hii itakuwa na athari yoyote katika biashara haramu ya siklaha hizo.