Barabara muhimu zafunguliwa Somalia

Image caption Inasemekana hali ya usalama ingali tete lakini angalau sio mbaya kama zamani kidogo

Barabara rasmi kutoka mji mkuu Mogadishu, kuelekea mji muhimu wa Kusini Magharibi mwa nchi Baidoa, umedhibitiwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika kutoka kwa wapiganaji wa kiisilamu.

Ni mara ya kwanza kwa barabara inayounganisha miji hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miaka miwili.

Muungano wa Afrika unasaidia serikali mpya ya Somalia kudhibiti eneo hilo kutoka kwa wapiganaji wa kiisilamu wa Al Shabaab.

Kundi hilo limelazimika kuondoka katika miji mikubwa lakini wangali wanadhibiti vijiji na maeneo mengi ya mashinani.

Sehemu ya mwisho ya barabara hiyo kutoka Mogadishu, ilidhibitiwa siku ya Jumatatu , kwa mujibu wa muungano wa Afrika ambao una majeshi 18,000 nchini humo.

Muungano huo ulisema kuwa hatua hii muhimu hairuhusu tu uhuru wa watu kutembea, lakini pia inafungua njia ya kusafirishia msaada wa kibinadamu.

Wakati huoho, mlipuko ulitokea mjini Mogadishu, katika ofisi ya Dahabshiil, moja ya kampuni kubwa za biashara ya kutuma pesa barani Afrika,

Mtu mmoja alijeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

Haijulikani aliyehusika na shambulio hilo lakini kampuni hiyo ilitishia kufunga ofisi zake katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab.

Licha ya shambulio hilo, hali imeimarika mjini Mogadishu tangu al-Shabab kuondoka mjini humo mwezi Agosti, , lakini wapiganaji wake wangali wanafanya mashambulizi ya kuvizia.