Afrika Kusini kuondoa wanajeshi 'CAR'

Image caption Rais Zuma amesema wanajeshi wake wataondoka Afrika Kusini baada ya serikali kupinduliwa

Afrika Kusini, inasema kuwa itawaondoa wanajeshi wake kutoka Jamuhuri ya Afrika ya Kati, baada ya waasi kupindua serikali zaidi ya wiki moja iliyopita.

Rais Jacob Zuma amesema kuwa mkataba kati ya nchi hizo mbili umetupiliwa mbali baada ya kung'olewa kwa rais Francois Bozize.

Bwana Zuma anakabiliwa na hasira za wananchi baada ya wanajeshi 13 wa nchi hiyo kuuawa katika mapinduzi ya kijeshi .

Alitoa tamko hilo katika mkutano wa dharura kuhusu mgogoro wa kisiasa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, ambao marais wa nchi za magharibi walikataa kumtambua kiongozi wa waasi kama rais wa taifa hilo.

Michel Djotodia alitangaza kuwa ataitawala nchi hiyo kwa kipindi cha mpito, baada ya kundi la waasi wa Seleka kuvamia mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, na kumaliza uongozi wa aliyekuwa rais Bozize, aliyetawala kwa mwongo mmoja.

Kiongozi huyo wa waasi amesema ataongoza nchi hiyo hadi uchaguzi utakapofanyika mwaka 2016.

''Haiwezekani kwetu kumtambua mtu aliyejitangaza kama rais,'' alisema rais wa Chad, Idriss Deby wakati wa mkutano huo.

Image caption Wanajeshi waliouawa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati wakati wa haratakati za mapinduzi

Alisema Zuma aliwaambia viongozi hao kuwa anapanga kuondoa majeshi yake nchini humo.

Afrika Kusini ilikuwa na takriban wanajeshi, 200 mjini Bangui, ambao kazi yao ilikuwa kujaribu kuzuia waasi wa Seleka kumng'oa mamlakani bwana Bozize ambaye kwa sasa yuko nchini Cameroon.

Pamoja na wanajeshi 13 kuuawa, wengine 27 walijeruhiwa, ikiwa idadi kubwa ya wanajeshi kuwahi kuuawa nje ya nchi hiyo tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Vifo hivyo vimesababisha tetesi nchini Afrika Kusini huku wakosoaji wakisema kuwa wanajeshi walipelekwa nchini humo ili kulinda maslahi ya kibiashara ya chama tawala.

Chama hicho hata hivyo kimekanusha madai hayo na kusema kuwa wanajeshi hao walikuwa wanatoa mafunzo kwa wanajeshi wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati pamoja na kulinda usalama.