Renamo wahusishwa na shambulio jengine

Maputo, Msumbiji

Watu waliokuwa na silaha wamewauwa watu wawili kati-kati mwa Msumbiji walipovamia basi na lori karibu na mji wa Muxungue wenye wafuasi wengi wa Renamo.

Basi hilo lilikuwa likisafiri kutoka mji mkuu, Maputo, kuelekea mji wa pili kwa ukubwa, Beira, lilipoviziwa na kushambuliwa.

Hili ni shambulio la kwanza dhidi ya basi lilobeba raia kwa kama miaka kumi.

Shambulio hilo limetokea siku mbili baada ya wanamgambo wa chama cha upinzani cha Renamo kuuwa askari polisi wane hukohuko Muxungue, ili kujaribu kuwafungua watu kadha waliokamatwa.

Msemaji wa Renamo, Osufo Madate, amekanusha kuwa chama chake kilihusika na shambulio dhidi ya basi na lori.

Msumbiji inakabili uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Vita baina ya serikali na Renamo vya miaka 16 vilimalizika katika miaka ya '90.