Uhuru Kenyatta, Rais mpya wa Kenya

Rais mpya wa Kenya Uhuru Kenyatta ameapishwa hii leo na kuchukua uongozi kutoka kwa Rais anayeondoka mamlakani Mwai Kibaki.

Hii ni baada ya Uhuru kumshinda Raila Odinga katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe nne mwezi Machi .

Wageni mashuhuri wakiweno marais wa nchi kadhaa za Afrika pamoja na wanadiplomasia na maelfu ya wananchi walishuhudia sherehe hizo katika uwanja wa michezo wa Kasarani viungani mwa mji wa Nairobi.

Odinga hakuhudhuria sherehe hizo baada ya jitihada zake kutaka mahakama ya juu zaidi kubatilisha matokeo ya uchaguzi kukosa kufua dafu.

Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC . Wanadaiwa kuwa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika miaka mitano iliyopita.

Wakati huo wawili hao walikuwa mahasimu wa kisiasa na wote wanakanusha madai dhidi yao.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir, ambaye mahakama ya ICC imetoa kibali cha kumkamata, kuhusiana na vita katika jimbo la Darfur, hakufika nchini Kenya kwa sherehe hizo licha ya kuwa alialikwa.

Kenyatta ni mwanawe rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, na amerithi mali nyingi sana .

Aidha Kenyatta ndiye rais mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuongoza nchi. Ana umri wa miaka 51 na ni mwanawe rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta.

Awali tulikuwa tunakusimulia kwenye ukurasa huu yaliyokuwa yanajiri shereha za kuapishwa kwa Uhuru ziliponoa nanga.

14:01 Rais wa Uganda ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki, Yoweri Museveni ahutubia wananchi na kumpongeza Kenyatta na naibu wake William Ruto, kwa ushindi wao na hata akawasifu wakenya kwa kuendesha uchaguzi kwa njia ya amani

13:25 Kenyatta akabidhiwa upanga na nakala ya katiba ya Kenya na rais mstaafu Mwai Kibaki ishara kuwa amekuwa amiri mkuu wa majeshi ya Kenya

13:21 Uhuru Kenyatta atawazwa rasmi kama rais wa Jamuhuri ya Kenya baada ya kukabidhiwa cheti kilichotiwa saini naye Rais mpya mwenyewe

13:01 Vigelegele na shangwe punde baada kuapishwa kwa Uhuru Kenyatta kama rais wa nne wa Kenya

12:59 Uhuru Kenyatta aapishwa kama rais mpya wa Kenya akiwa kando yake akiwa na mkewe Margaret Kenyatta

12:58 Uhuru Kenyatta ajiandaa kula kiapo chake

12:56 Jaji Mkuu wa Kenya Willie Mutunga amtambulisha rais mteule wa Kenya kwa wakenya kuambatana na sheria na matakwa ya katiba ya Kenya na kuchukua kiapo cha kushuhudia kuapishwa kwa Uhuru Kenyatta

12:23 Rais Mwai Kibaki anayeondoka madarakani anakagua gwaride la heshima

12:03 Victor Otieno kupitia facebook akiwa Nairobi anamshauri Uhuru kuwa amekosolewa na watu wengi kuwa hawezi kuwatekelezea wakenya mahitaji yao. Sasa natoa changamoto kwake kuwa afanye kazi na aweze kuwaonyesha kuwa maoni yao sio sawa na ahakikishe kuwa katiba inatekelezwa kikamilifu.

11:45 Shangwe na vigelegele akiwasili rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta

11:45 Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn,pamoja na wageni wengine waheshimiwa wawasili katika uwanja wa Kasarani akiwemo Rais mstaafu Daniel Moi.

11:35 Naibu rais mteule William Ruto aliwasili na mkewe