Korea Kusini yaimarisha ulinzi wake

Image caption Mtambo wa Korea Kusini wa kukinga mashambilizi ya makombora

Korea Kusini imeimarisha hali yake ya tahadhari kufuatia habari kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la kombora lake moja la masafa ya kadiri.

Marekani na Korea Kusini zinasema kuwa hadi kufikia sasa wanazo habari kwamba mojawapo ya kombora lililo na uwezo wa kushambulia umbali wa kilomita 3,000 ambalo halijafanyiwa jaribio limejazwa mafuta tayari kulipuliwa.

Mwandishi wa habari wa BBC mjini Seoul anasema kwamba ingawa kufanya jaribio la kombora hilo ni ishara ya uchokozi na ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa lakini haliwezi kubabaisha kijeshi kwa njia yoyote; pengine tu shughuli yenyewe ipatwe na kasoro.

Japan kwa upande wake imeweka zana na kukabiliana na makombora katika mji mkuu wa Tokyo.

Pyongyang imekuwa ikitoa vitisho dhidi ya kambi za kijeshi za Korea Kusini, Japan na Marekani.

Vitisho hivyo vinakuja baada ya vikwazo vipya na vikali zaidi kutolewa dhidi ya Korea Kaskazini mwezi jana kufuatia jaribio lake la tatu la kinuklia.

Mbali na hayo, uchunguzi wa hapo awali uliofanywa na Korea Kusini kuhusu uvamizi wa mtandao, mwezi jana na ambao uliathiri idadi kubwa ya benki na mitambo ya kupperusha matangazo umeonyesha kuwa wa kulaimiwa kwa hilo ni Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini inaaminika kukamilisha mipango yake ya kuzindua kombora baada ya kuhamisha makombora yakemawili upande wa Pwani mwa nchi.

Ili kujibu tisho hilo, Korea Kusini kwa ushirikiano na Markani zimeimarisha mitambo yake ya kuchunguza shambulio lolote.

Korea Kaskazini ilizindua Kombora lake wakati wa gwaride la jeshi mwaka 2010 lakini bado haijalifanyia jaribio lolote.

Jaribio hilo linaweza kufanyika wakati wowote kuanzia sasa , kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Yun Byung.