Korea na Syria kwenye agenda ya G8

Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Uingereza wakiwasili kwenye mkutano wa G8

Migogoro ya Syria na Korea ndiyo itakuwa swala kuu katika agenda ya mkutano wa nchi za G8 , baadaye hii leo mjini London Uingereza.

Duru zinasema kuwa Japan, inayoshiriki mkutano huo, inatafuta kauli kali ambayo itaungwa mkono na nchi zote za G8 kuhusu Korea

Korea Kaskazini imekuwa ikitoa vitisho dhidi ya kambi za kijeshi za Korea Kusini, Japan na Marekani katika eneo hilo.

Mawaziri wa mambo ya nje pia watajadiliana kuhusu mzozo wa Syria baada ya kukutana na viongozi wa upinzani Jumatano.

Mwandishi wa BBC wa maswala ya kidiplomasia, James Robbins , anasema kuwa mawaziri wanakubaliana kuwa vitihso vya kivita kutoka Korea Kaskazini pamoja na maandalizi ya kufanya jaribio la makombora ni vitisho vibaya sana

''Marekani ina msimamo mmoja na sisi kuhusu Korea Kaskazini ,'' waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema kwenye mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Korea Kusini imetahadhari pakubwa huku kukiwa na dalili kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la kombora lake mpya.

Pyongyang imehamisha makombora mawili pwani mwa nchi. Makombora hayo yanaweza kwenda umbali wa kilomita 3,000.

Inaarifiwa kuwa huenda kombora hilo likazinduliwa Jumatatu ambayo itakuwa siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taifa hilo Kim Il-sung

Korea Kaskazini imeanza kutoa vitisho vipya baada ya kuwekewa vikwazo vipya na Umoja wa Mataifa kufutia hatua yake ya jaribio la tatu la nuklia