Idadi ya waliofariki yaongozeka Somalia

Takriban watu 28 wameuawa katika shambulio la bomu na risasi mjini Mogadishu Somalia.

Wengine hamsini wakiwemo washambuluaji tisa pia wanasemekana kuuawa baada ya mtu aliyekuwa amejihami kuvamia majengo ya mahakama na kuanza kushambulia watu kiholela.

Baadaye bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari lilipuka kando ya barabara inayoelekea katika uwanja wa ndege ambako wafanyakazi wawili wa misaada wa Uturuki walikuwepo

Kundi la wapiganaji la al-Shabab linasema ndilo limefanya shambulio hilo.

Al-Shabaab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, limelaumiwa kwa mashambulio kadhaa mjini Mogadishu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Lakini wadadisi wanasema kuwa mashambulizi yaliyotokea hapo jana ndio mabaya zaidi kushuhudiwa tangu wapiganaji wa Al Shabaab kufukuzwa Mogadishu mwaka 2011.

Sasa shambulio hilo limesababisha hali ya hofu miongioni mwa wakaazi wa Mogadishu.

Sio eti ni mashambulizi makubwa kuwahi kushuhudiwa Mogadishu , bali yametokea huku wakaazi wa Mogadishu ukianza kuwa mji wenye utulivu.

Mashambulizi hayo bila shaka yatakuwa changamoto kubwa kwa serikali katika mji mkuu. Polisi wamepelekwa katika miji mikubwa ili kutoa ulinzi kwa majengo ya serikali.

Lakini serikali katika siku za nyuma ilikubali kuwa inaweza tu kufanya kadri ya uwezo wake kujaribu kuzuia washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Vifo vya wafanyakazi wa misaada kutoka Uturuki, pia vitazua wasiwasi miongoni mwa idadi inayoongozeka ya mashirika ya misaada inayofanya kazi Somalia.