16 wafariki kwa kuangukiwa na mgodi Ghana

Image caption Ghana ni moja ya nchi kubwa Afrika ambazo huzalisha dhahabu

Takriban watu 16 wamefariki baada ya kuangukiwa na mgodi ambao ulikuwa hautumiki nchini Ghana.

Maafisa wanasema kuwa kulikua na maporomoko ya ardhi katika sehemu ambayo ilikua haitumiki karibu na mji wa Kyekyewere ambao una sifa ya kuwa na wachimbaji haramu wa migodi.

Waokoaji waliondoa miili 16 baada ya mgodi huo kuporomoka siku ya Jumatatu , kwa mujibu wa maafisa wakuu.

Haijulikani idadi ya watu waliokuwemo ndani ya mgodi huo , lakini inaarifiwa kuwa hukana dalili kuonyesha kuwa bado kuna miili mingine ndani ya mgodi huo.

Ghana ni moja ya nchi kubwa zenye kuzalisha dhahabu hasa baada ya kujulikana kama pwani ya dhahabu.

Afisaa mmoja aliambia shirika la habari la Reuters kuwa mchimbaji mmoja aliyekuwa amejeruhiwa alifariki baadaye hospitalini. Hii inaongeza idadi ya waliofariki hadi 17.

Uchimbaji haramu ni swala linalotela wasiwasi mkubwa nchini Ghana hasa katika maeneo ambako wachimbaji hutumia vifaa vya kisasa kwa shughuli zao.

"ni mgodi ambao ulikuwa hautumiki rasmi ingawa hutumiwa sana na wachimbaji haramu,'' alisema afisaa huyo Owusu-Ashia.

Aliongeza kuwa licha ya uhamasisho mkubwa wa watu kutochimba kiharamu, shughuli hizo bado huendelea kufanywa.

Zaidi ya rais 120 wa China walikamatwa kama sehemu ya harakati za kukomesha uchimbaji haramu.