Mkwe wa rais wa zamani Tunisia apata hifadhi

Mkwe wa aliyekuwa rais wa Tunisia amepata hifadhi nchini Seychelles.

Sakher El Materi ambaye ni mfanyabiashara, alikamatwa alipokuwa akijaribu kuingia nchini humo mwaka jana na kisha akaomba hifadhi mwezi Februari.

Alitoroka Tunisia kwenda Qatar baada ya mapinduzi ya kiraia yaliyomng'oa mamlakani aliyekuwa rais Zine al-Abidine Ben Ali mwezi Januari mwaka 2011.

Miezi kadhaa baadaye mahakama ilimhukumu kwa kosa la ufisadi bila yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.

Materi, pamoja na mkewe na watoto wao watatu wamepewa hifadhi ya mwaka mmoja kulingana na maafisa wa uhamiaji kisiwani humo.

Kisiwa hicho, kilikuwa sehemu ya likizo kwa familia ya rais na jamaa zake wa karibu.

Sheria ya nchi hiyo haitoi nafasi kwa wageni kupewa hifadhi ya kisiasa , kulingana na afisaa mmoja wa serikali.

Lakini alipewa fursa hiyo kwa sababu inaaminika kuwa Materi asingetendewa haki nchini Tunisia.

Materi pia alipatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi na kuhukumiwa bila ya yeye kuwepo mahakamani pamoja na mkewe Nesrine, na babake ambaye aling'olewa mamlakani.

Wawili hao walihukumiwa miaka 16 jela huku Nesrine akipokea miaka minane jela.