Watoto waathirika zaidi na vita (CAR)

Haki miliki ya picha
Image caption Maeneo wanayopigania waasi wa Seleka

Shirika la kuwahudumia watoto la umoja wa mataifa UNICEF, limeelezea hofu ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaouawa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

UNICEF linasema kuwa watoto hao wanajipata katika maeneo ya vita wakati makundi yaliyojihami yanapopambana viwanjani na hata makanisani.

Aidha shirika hilo limesema kuwa takriban watoto watatu waliuawa na wengine zaidi ya ishirini kujeruhiwa vibaya siku ya ijumaa.

Linadai kuwa watoto hao wamesajiliwa kama wapiganaji katika makundi ya waasi.

Kumekuwa na mapigano pamoja na uporaji katika mji mkuu Bangui baada ya waasi kuuteka mji mkuu mwezi jana.

Wiki tatu baada ya waasi wa Seleka kutwaa mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi,uporaji na ghasia zimekithiri nchini humo watoto wakiwa katika hatari kubwa zaidi.

Tangu makabiliano kuanza upya mwishoni mwa mwezi wa Machi, watoto wengine wengi zaidi wamekuwa waathiriwa wa risasi wakati wengine wakisajiliwa kama wapiganaji. Pia kumekuwa na taarifa za kuongezeka kwa visa vya ubakaji

“Tunaiona nchi hii ikikumbwa na ghasia huku watoto wakiwa waathiriwa wakubwa,'' alisema Souleymane Diabate afisaa mkuu wa shirika hilo katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati. ''Ghasia dhidi ya watoto lazima zisitishwe. Watu wasio na hatia wanauawa au kujeruhiwa na lazima zichunguzwe na maafisa wakuu,'' alisema Biabate

Wiki jana UNICEF ilitoa vifaa muhimu vya matibabu na hata kuweka kliniki ya muda kwa akina mama wajawazito ndani na nje ya mji wa Bangui. Watoto waliojeruhiwa pia wamepokea matibabu