Mahakama yaamuru Pervez Musharaf akamatwe

Mahakama nchini Pakistan imeamuru kukamatwa kwa aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini humo Pervez Musharraf kuhusiana na hatua yake ya kutaka kuwapa kifungo cha nyumbani majaji mwaka 2007.

Bwana Musharraf alikuwepo katika mahakama ya juu zaidi mjini Islamabad wakati majaji walipotoa kibali cha kumkamata.

Amekuwa akiomba mahakama kuongeza muda wake wa dhamana.

Polisi waliokuwepo mahakamani hawakumkamata wakati mahakama ilipotoa kibali hicho.

Generali huyo wa zamani aliondoka mahakamani mara moja akisindikizwa na walinzi wake.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa licha ya sheria inayowazuia polisi kumkamata mtu katika sehemu ya mahakama, washukiwa kawaida hufungwa pingu

Hata hivyo, Bwana Musharraf anaweza kukata rufaa dhidi ya kibali hiki cha kumkamata.

Masaibu ya kisiasa

Musharaf alirejea Pakistan baada ya kuishi nje ya nchi hiyo kwa miaka mingi mwezi jana, akitumai kuwa kiongozi wa chama chake cha (APML) katika uchaguzi mkuu ujao.

Lakini mapema wiki hii, hatua yake ya kujitosa kwenye siasa ilikataliwa na eneo la Chitral, moja ya maeneo bunge manne aliyotaka kuwania.

Tayari alikuwa amekosa nafasi ya kugombea viti vingine vitatu. Mawakili,wake wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama.

Musharaf anakabiliwa na kesi kadhaa na amekuwa akikwepa kukamatwa tangu kurejea kwake nchini humo, pamoja na njama ya kutaka kumfungulia kesi ya uhaini.

Kundi la Taliban pia limeahidi kumuua maksudi rais huyo wa zamani aliyechukua mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi mwaka 1999.

Anakabiliwa na kesi kadhaa, zinazohusiana na wakati alipokuwa mamlakani huku nyingine ikihusu mauaji ya Benazir Bhutto mnamo mwaka 2007 pamoja na kiongozi mwingine wa kikabila kutoka eneo la Balochistan.

Ametaja kesi zote dhidi yake kama zisizo na msingi na ambazo zinashinikizwa kisiasa.

Duru zinasema kuwa jeshi la Pakistan lenye nguvu sana na ambalo aliliongoza tangu mwaka 2007 halijaingilia kivyovyote kumzuia kuporomoka kisiasa.

Licha ya mstakabali wake kuonekana tete, wachache wanaamini kuwa jeshi linaweza kuruhusu mtu aliyewahi kuwaongoza kufungwa jela au kuuawa na wapiganaji wa kiisilamu.

Hata hivyo ripoti zinasema kuwa bado anaweza kukamatwa na kuzuiliwa kwake karibu na mji wa Islamabad, alikokwenda baada ya kuondoka mamlakani.