Israel sharti izuie silaha kwenda Syria

Image caption Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema, Israel ina haki ya kuzuia silaha kuishia kwenye mikono ya wapiganaji wa kiisilamu nchini Syria.

Akiongea na BBC, Bwana Netanyahu ameonya silaha za kudungua ndege na makombora zinaweza kubadilisha mashariki ya kati na kuifanya uwanja wa magaidi na kuhatarisha usalama wa dunia.

Bwana Netanyahu yuko mjini London wakati Uingereza inapendekeza marufuku ya silaha iliyowekewa Syria na bara Ulaya kuondolewa. Uingereza inataka wapiganaji nchini Syria kupokea silaha.

Japo Netanyahu anaunga mkono hatua hiyo, anaonya huenda silaha zikaishia kwenye mikono ya wanamgambo wa kiisilamu na kuhatarisha hali zaidi ya ilivyo kwa sasa.

Amesema wasi wasi wa Israel ni silaha zilizoko ndani ya Syria, zikiwemo makombora ya kudungua ndege ambayo ni hatari endapo yataishia kwenye mikono ya magaidi.

Waziri Mkuu wa Israel hata hivyo amesema nchi yake haina mpango wa kushambulia Syria, japo amesisitiza kua Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya mashamblizi.

Israel ina wasi wasi kuhusu kundi la Nusra Front liliko Syria na ambalo limekiri kua na uhusiano na mtandao wa Al Qaeda. Netanyahu amesema wasi wasi wake siyo kwa Israel pekee bali ni kwa dunia nzima.