Uokozi ni mgumu kwenye tetemeko Uchina

Wafanya kazi za uokozi wamekuwa wakipata shida kufika kwenye vijiji vya mbali milimani vilioko kusini-magharibi mwa Uchina, baada ya tetemeko la ardhi ambalo linalijulikana kuuwa watu 200 na kujeruhi zaidi ya 11,000.

Wanajeshi 17,000 wametumwa huko kwenda kusaidia.

Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi asubuhi karibu na mji wa Ya'an katika jimbo la Sichuan.

Waokozi wamekuwa wakijaribu kupanda barabara nyembamba zilizozongwa na maporomoko.

Lori moja la jeshi lilobeba wanajeshi 17 lilipinduka mlimani na kumuuwa mwanajeshi mmoja na kujeruhi wengine saba.

Magari ya kubeba wagonjwa yanawapeleka manusura katika kituo kwenye hospitali kuu mjini Ya'an.

Majeruhi wengi, baadhi yao wamevunjika viungo, wanatibiwa kwenye mahema yaliyowekwa nje ya hospitali.

Tetemeko hili lilikuwa ni dogo likilinganishwa na lile la mwaka 2008 ambalo liliuwa watu 70,000.

Lakini kwa sababu ya shida za kuwafikia manusura na vitetemeko vidogo vinavoendelea wakati wote, idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.