Israel yaituhumu Syria kutumia silaha za kemikali

Image caption Mizoga ya wanyama ambao wenyeji wanasema wameuawa na silaha za kemikali

Kwa mara ya kwanza kabisa Israel imeituhumu Syria hadharani kuwa inatumia silaha za kemikali kupigana dhidi ya waasi nchini humo.

Mkuu wa idara ya utafiti wa kijasusi nchini Israel Brigadier Itai Baron ameliambia kongamano kuhusu usalama kwamba silaha hizo zimetumika mara kadhaa , ikiwa ni pamoja na shambulizi lililotekelezwa tarehe kumi na tisa mwezi uliopita wa Machi, ambalo maafisa wa Syria walisema lilitekelezwa na wanamgambo.

Amesema silaha hizo za kemikali huenda zinajumuisha sumu hatari ya Sarin.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutumika mrundiko wa silaha za kemikali zilizopo nchini humo katika mzozo uliopo nchini humo ambao unaingia katika mwaka wake wa tatu.