Makabiliano makali mkoani,Xinjiang China

Serikali katika mkoa wenye mzozo wa Xinjiang nchini China, imesema mapigano yamesababisha vifo vya watu 21 wakiwemo polisi 15 na maafisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye tovuti rasmi ya serikali ya Xinjiang, mapigano hayo yametokea Jumanne mchana katika wilaya ya Bachu Kashgar.

Mapigano hayo yalianza baada ya maafisa kufanya upekuzi majumbani kwa lengo la kusaka silaha. Wafuasi sita wa genge moja la kihalifu ni miongoni mwa waliouawa.

Kumekuwa na mapigano ya hapa na pale katika mkoa wa Xinjiang katika miaka ya hivi karibuni.

Matukio hayo yamekuja wakati kukiwa na hali tete kati ya jamii ya Waislamu wa Uighur na wale wa jamii ya Hans Chinese. Mwaka 2009, takriban watu 200 wengi wa jamii ya Hans waliuawa baada ya kutokea mapigano mabaya.

Mwandishi wa BBC, Celia Hatton, amesema ni vigumu kuthibitisha taarifa kutoka Xinjiang.

Waandishi wa habari wa kigeni wanaruhusiwa kufika katika mkoa huo, lakini mara nyingi wamekuwa wakitishiwa na kunyanyaswa pale wanapojaribu kuthibitisha habari za machafuko ya kikabila ama vurugu zinazopangwa dhidi ya mamlaka ya serikali.

Idara za propaganda za China zimevionya vyombo vya habari vya ndani dhidi ya kuandika zenyewe habari za masuala nyeti ya Xinjiang na kuviamuru kuandika zile habari rasmi zinatolewa na vyombo vya habari vya serikali.

Kwa mujibu wa taarifa mapigano hayo yaliibuka baada ya maafisa kuelezea kuwa ni wafanyakazi wa serikali kufanya upekuzi wa kusaka silaha majumbani na kasha kutekwa nyara.

Imeongeza kuwa, wafuasi wengine nane wa genge la kihalifu walikamatwa na kulielezea tukio hilo kuhusishwa na ugaidi. Hata hivyo hakuna taarifa za kutambuliwa kwa wahalifu hao.

Maafisa kumi na polisi waliouawa walikuwa wa jamii ya kabila la Uighur. Jamii hiyo katika mkoa wa Xinjiang inachangia 45% ya idadi ya watu lakini kuwasili kwa watu wa jamii ya Hans kumepunguza ushawishi wa utamaduni wao wa asili.

Watawala jijini Beijing mara nyingi wamekuwa wakiwashutumu watu wa Uighur wenye msimamo mkali kwa kuhusika na machafuko ya Xinjiang wanaotaka mkoa huo ujitenge.

Nao wanaharakati wa Uighur wanaishutumu Beijing kuzidisha vitisho ili kuhalalisha utawala wa mabavu.