Je unawakumbuka Kriss Kross?

Image caption Chris Kelly

Chris Kelly, mmoja wa wasanii wa kilichokuwa kikundi cha vijana wawili waimbaji wa muziki wa kizazi kipya, mapema miaka ya tisini, Kris Kross, amefariki hospitalini mjini Atlanta akiwa na umri wa miaka 34.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari Kelly alipatikana kwake siku ya Jumatano akiwa hapumui.

Kelly, aliyejulikana kama "Mac Daddy", na mwenzake Chris "Daddy Mac" Smith wanasifika kwa kibao chao cha 'Hit Jump' walichokipiga mwaka 1992.

Mnamo mwezi Februari walifanya tamasha la kusherehekea miaka 20 ya kampuni iliyokuwa inatengeza muziki wao.

Wasanii hao walisifika kwa kuvaa long'i zao zikiwa zimelegea sana wakati walipokuwa na umri wa miaka 13 ambapo pia ndipo waligunduliwa katika duka moja kubwa mjini Atlanta.

Polisi walifika katika nyumba ya Kelly, Jumanne saa kumi na nusu jioni alipopelekwa hospitalini ingawa alisemekana kufariki alipofikishwa hospitalini.

Hata hivyo hapakuwa na habari zozote kuhusu sababu ya kifo chake. Matokeo ya uchunguzi utakaofanywa Alhamisi yatatolewa baadaye.

"inaonekana kama huenda alikuwa ametumia kiwango kikubwa cha dawa kupita kiasi,'' alisema msemaji mmoja wa polisi.

Kibao cha Jump ndicho kilikuwa cha kwanza cha waimbaji hao na ambacho kilikuwa maarufu zaidi kuliko vyote na ndicho pia kiliwapa umaarufu wao.

Kris Kross baadaye walitoa albamu yao iliyosifika kamaTotally Krossed Out, na walifanya ziara na mwenda zake Michael Jackson.

Licha ya kutoa vibao vingine mashuhuri kama Warm It Up na Tonite's tha Night, havikuweza kutoa ushindani kwa kibao chao cha kwanza.

Kris Kross walitoa albamu zingine mbili miaka ya tisini kabla ya wawili hao kuachana, kila mtu akiimba kivyake.

Mnamo mwaka 2009 ripoti zilijitokeza kuwa Kelly alikuwa anaugua Saratani lakini alikanusha madai hayo na kusema kuwa alikua tu anaugua ugonjwa wa Alopecia.

"afya yangu ni nzuri, alisema wakati alipohojiwa kwenye televisheni.''