Ghasia zaendelea mjini Conakry, Guinea

Watu kama watatu wameuwawa nchini Guinea katika mapambano baina ya polisi na waandamanaji waliodai uchaguzi huru na wa haki.

Ghasia zimekuwa zikiendelea kwa siku ya pili katika mji mkuu, Conakry.

Afisa mmoja wa upinzani alieleza kuwa waliokufa walikuwa wafuasi wa upinzani.

Upinzani nchini Guinea unasema Rais Alpha Conde hakuwashauri kabla ya kutangaza siku ya uchaguzi wa wabunge kuwa tarehe 30 Juni.

Upinzani unataka wafuasi wake wafanye maandamano hadi rais afute uchaguzi huo.

Rais Conde alishika madaraka mwaka wa 2010 baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia tangu mwaka 1958.

Lakini uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanywa mwaka wa 2011 umekuwa ukiahirishwa kwa sababu wanasiasa wameshindwa kuwafikiana.