Bomu lauwa watu kadha Mogadishu

Watu kama saba wameuwawa na wengine kadha kujeruhiwa katika shambulio la kujitolea mhanga mjini Mogadishu, Somalia.

Mwandishi wa BBC aliyefika katika tukio hilo ambapo mtu aliyetega bomu kwenye gari alijiripua, anasema mripuko mkubwa uliharibu majengo yaliyo karibu.

Wakuu walisema gari la serikali lilobeba wafanyakazi za usaidizi lililengwa.

Barabara kuu mjini Mogadishu zilifungwa tangu Jumatano kwa sababu wakuu walionya kuna shambulio lilopangwa na wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Al Shabab.

Barabara hizo zilifunguliwa Jumamosi.

Mashambulio ya kujitolea mhanga hutokea mara kwa mara mjini Mogadishu.