Rafsanjani awania kugombea urais Iran

Rais wa zamani wa Iran, Ali Akbar Hashemi Rafsanjani, amejiandikisha kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao.

Bwana Rafsanjani mwenye umri wa miaka 78 aliandikisha jina lake dakika chache kabla ya muda kumalizika wa kupeleka maombi.

Mwandishi wa BBC anasema Bwana Rafsanjani ni mpinzani wa viongozi wa msimamo mkali walio karibu na kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Mpatanishi mkuu katika mazungumzo kuhusu mradi wa nuklia wa Iran, Saeed Jalili, piya amependekeza jina lake.

Rais anayeondoka madarakani, Mahmoud Ahmadinejad, ameshatumika mihula miwili na hawezi kugombea tena urais.

Wagombea urais watachujwa na halmashauri maalumu, Guardians Council, kabla ya kuruhusiwa kusimama katika uchaguzi.