Mateka wa Red Cross waachiliwa Yemen

Image caption Visa vya utekaji nyara hutokea sana nchini Yemen

Watekaji nyara Kusini mwa Yemen, wamewaachilia wafanyakazi watatu wa shirika la Msalaba mwekundu pamoja na mkalimani wao mwenye uraia wa Yemen.

Wafanyakazi hao wa kigeni, raia wa Uswizi, Mkenya na Mmisri, walitekwa nyara siku ya Jumatatu mjini Jaar katika mkoa wa Abyan.

Kuachiliwa kwa watatu hao kunakuja baada ya viongozi wa kijamii kuwaomba watekaji nyara hao kuwaachilia.

Visa vya utekaji nyara wa wafanyakazi wa kigeni, ni kawaida kutokea nchini Yemen.

Watu kutoka makabila fulani wanasifika kwa kuwateka watu nyara kwa lengo la kutaka serikali kuwashughulikia malalamiko yao.

Lakini wapiganaji kutoka kundi la kigaidi la al-Qaeda, pia wamekuwa wakidai kutekeleza baadhi ya visa hivyo.

Mapema mwezi huu, wanandoa wawili kutoka Finland walitekwa nyara mwezi Disemba na kisha kuachiliwa. Mnamo mwezi Februari mwalimu mwenye uraia wa Uswizi aliachiliwa na watekaji nyara baada ya kuzuiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.