Ajali ya mgodi watu 20 wafariki Congo

Image caption Ramani ya DRC

Zaidi ya watu 20 wamefariki dunia wakati mgodi mmoja uliporomoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mamlaka za Congo zinasema mgodi huo ulioko karibu na kijiji cha Rubaye katika mji wa Masisi Kaskazini mwa jimbo la Kivu uliporomoka siku ya Alhamisi Asubuhi.

Meya wa Masisi, Dieudonne Shishuku ameiambia BBC kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.

Amesema bado wanasubiri waokoaji maalumu wa vifaa vya kufukua ardhini waanze kazi ya ukoaji ambapo mgodi huo unakadiriwa kufikia mita 30 kwenda chini.

Shughuli zote za uchimbaji wa madini zimesimamishwa mjini humo.

Kumekuwa na shughuli za uchimbaji haramu wa madini kwenye mji huo ambao una utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, madini ya chuma na coltan yanayotumiwa kwa simu lakini eneo hilo limekuwa na mapigano ya muda mrefu. Faida inayotokana na mauzo ya madini nchini humo, yanaaminika kuchangia pakubwa katika mzozo unaokumba Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wakiwa masikini.