Drogba atemwa na kocha wa Ivory Coast

Image caption Didier Drogba

Aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast na nyota wa Chelsea, Didier Drogba, ameachwa nje ya kikosi kitakachoakilisha Ivory Coast kwenye mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Gambia na Tanzania.

Hii ni mara ya pili mtawalia kwa kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi kumuacha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka Thelathini na Tano.

Mchezaji huyo hakuonyesha mchezo mzuri wakati wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini hatua iliyomlazimisha kocha huyo kumuacha nje ya kikosi chake kilichocheza na Gambia mwezi Machi mwaka huu.

Mlinda lango wa Manchester City, Kolo Toure, vile vile ameachwa nje ya kikosi hicho cha wachezaji 26.

Lamouchi alisema uamuzi huo ni changamoto kwa Drogba kuimarisha mchezo wake ili aweze kujipa nafasi katika timu hiyo ya taifa.

''Drogba ni mchezaji wa kimataifa na mwenye hadhi kuliko mchezaji yeyote wa timu ya taifa, lakini amekuwa na matatizo katika kipindi cha miezi minane iliyopita'' Alisema Lamouchi.

Dalili za Drogba kustaafu?

Image caption Kolo Toure ambaye pia ametemwa nje

Licha ya kocha huyo kusisitiza kuwa Drogba, angali na nafasi ya kucheza mechi za kimataifa, wengi wataanza kujiuliza ikiwa mshambuliaji huyo atapata fursa ya kuongeza idadi ya mechi alizocheza na timu hiyo ya taifa, kutoka tisini na sita hasa kutokana na hali yake kwa sasa baada ya kuisaidia klabu yake ya Galatasaray kunyakua kombe la ligi kuu ya soka nchini Uturuki.

Kocha huyo amewaita Romaric N'Dri Koffi, anayeichezea klabu ya Real Zaragoza, nchini Uhispania na Jean-Jacques Gosso, anayeichezea klabu ya Mersin Idman Yurdu ya Uturuki.

Kuna wachezaji wawili wapya katika kikosi hicho, Mlinda lango Serge Aurier wa klabu ya Toulouse na mshambulizi Mathis Bolly anayeichezea Fortuna Duesseldorf ya Ujerumani.

Ivory Coast inachuana na Gambia tarehe nane mwezi ujao na Tanzania siku nane baada mjini Dar Es Salaam.

Ivory coast inaongoza katika kundi lao na alama moja mbele ya Tanzania. Morocco ina alama mbili huku Gambia ikiwa mkiani na alama moja katika kundi hilo la C.