Wafyatuliwa risasi za mipira mgodini A.Kusini

Image caption Uhusiano kati ya wafanyakazi na wamiliki wa migodi umedorora

Wachimba migodi kumi wamejeruhiwa nchini Afrika Kusini baada ya walinzi kuwafyatulia risasi za mipira wafanyakazi wa migodini. Taarifa hii ni kwa mujibu wa duru za polisi.

Msemaji wa polisi Thulani Ngubane amesema kuwa wachimbaji migodi hao tayari wamepelekwa hospitalini.

Msemaji wa kampuni ya Lanxess, inayomiliki mgodi wa Chrome mine, alisema kuwa polisi waliwafyatua risasi hizo kama njia ya kujilinda.

Uhusiano kati ya wafanyakazi na wamiliki wa migodi umedorora hasa baada ya polisi kuwaua wafanyakazi 34 wa migodini katika mgodi wa Marikana mwaka jana.

Wiki jana wafanyakazi katika kampuni ya Lonmin waligoma kwa siku mbili.

Wachimba mgodi wa Lanxess chrome, walifanya mgomo ambao haukuwa umepangwa baada ya kutofautiana na waajiri wao kuhusu marupurupu yao.

Inaarifiwa kuwa hali imetulia baada ya kufyatuliwa riusasi za mipira katika mgodi wa Rustenburg Kaskazini mwa Johannesburg, na kuwa hakuna yeyote miongoni mwa waliojeruhiwa yuko katika hali mbaya.