Wanavyoandamwa na Ukeketaji Uingereza

Ukeketaji au kukatwa kwa sehemu za siri za mwanamke , inadhaniwa kuwaathiri angalau wanawake 66,000 nchini Uingereza.

Mara nyingine kitendo hiki hufanyika kwa wasichana ambao hurejeshwa nyumbani kwa jamaa zao Afrika Mashariki, lakini pia inaaminika kuwa wanawake wanakeketwa nchini Uingereza pia.

Hata hivyo hakuna hatua zozote za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wanaotenda unyama huo lakini serikali inasisitiza kuwa iko tayari kuhakikisha kuwa ukeketaji unakwisha.

Hospitali kadhaa na kiliniki za kijamii mjini London, huwasaidia wanawake ambao wamekeketewa. Pia kuna kliniki moja Birmingham na nyingine inatarajiwa kufunguliwa Bristol.

Moja ya kliniki za serikali katika hospitali yaChelsea, huwatibu zaidi ya wanawake 100 kila mwaka ambao wamekeketwa na kuwashona kwa sababu ya imani za kitamaduni, akiwemo Filsan, mwenye umri wa miaka 35.

Filsan ni mama mwenye watoto watatu na anaishi nchini Uingereza . Alikabidhiwa nguo mpya akiwa tu na umri wa miaka saba , ikiwa ni dalili ya muda kuwadia wa yeye kukeketwa.

"wasichama wamekuwa wakikeketwa kisiri nchini humu, lakini huu ni unyanyasaji wa wanawake na watoto.''

'miguu kufungwa pamoja'

''Nilihisi uchungu mwingi, licha ya kudungwa sindano ya kumaliza uchungu. Wakati uchungu ulipokwisha, singeweza hata kwenda haja ndogo.''

"tulilazimika kulala sakafuni , kwa sababu hata hatungeweza kutembea. Miguu yetu ilikuwa imefungwa kwa kamba, kwa hivyo hatungeweza kuitenganisha , yaani uchungu ulikuwa mwingi sana.

"na sasa ikafika muda wangu kujifungua mwanangu wa kwanza. Nilichokuwa nakitafakari tu, je mtoto anaweza kupitia vipi katika sehemu ambayo imeharibiwa hivyo?

''Ilikuwa hali ngumu sana kwangu.Kutafakari yote niliyoyapitia, lakini kwa sasa nina afueni kwa sababu nilikuwa na daktari mzuri ambaye aliweza kuelewa kila kitu nilichokuwa napitia.''

Kumbu kumbu za Filsan humletea majonzi tele. Lakini jazi yake anayoifanya na shirika moja la kisomali, inampa matumaini kwa sababu anahisi kuwa watu wa jamii yake wameanza kupinga ukeketeaji.

Anasema kuwa watu wanafahamu na kuelewa kuwa sio kitendo kizuri na kuwa kinahitaji kukomeshwa.

Inasemekana kuwa zaidi ya wasichana 20,000, walio chini ya umri wa miaka 15 , huwa katika hatari ya kukeketwa kila mwaka nchini Uingereza.

Wanawake 66,000 nchini Uingereza wanaishi na athari na makovu ya ukeketeji.

Hakuna manufaa yoyote ya kiafya yanatokana na ukeketaji, bali wanawake huharibiwa sehemu zao za siri bure.

''Kazi nyingi inafanywa barani Afrika, lakini lazima tuwahamasishe watu ikiwemo jamii kila sehemu ambazo zinakumbatia utamaduni wa kuwakeketa wanawake,'' anasema Filsan

Tangazo maalum la kibiashara limepeperushwa kwenye stesheni moja ya kisomali na hivyo kuchochea idadi kubwa ya watu wanaopiga simu katika kniliki ya Queen Charlotte's.

Mkunga Juliet Albert, alielezea kwa nini baadhi ya familia hulazimu wasichana wao kukeketwa.

Anasema ''wanawake wengi, husema kuwa hawatakubali kufanyiwa kitendo hiki , lakini kwa sababu ya shinikizo za kimila na kitamaduni kuhusiana na ukeketeji, hawezi kukwepa.

Baadhi ya wanawake huwa na wasiwasi kuwa ikiwa wasichana wao hawatafanyiwa kitendo hicho, jamii itawatenga na kuwa hawawezi kuoleka tena.

Wao hupata matayizo mengi ya kiafya kutokana na kufanyiwa ukeketaji, kama magonjwa , uchungu wakati wa kujifungua au hata wakati wanapokuwa wanajamiiana na waume zao.

Na tunachokifanya ili kurekebisha tatizo hilo ni kushona na kuacha shimo ndogo wanayotumia kujifungulia mtoto na kujamiiana.''

Kliniki hii huwaelekeza wasichana na wanawake kwa wahudumu wa kijamii ikiwa wanahisi kuwa yeyote anakabiliwa na tisho la kukeketwa.

Waziri wa afya Anna Soubry anasifu hatua hii sana

Bi Soubry anasema kuwa wanawalinda watoto wote nchini humo licha ya wanavyotaka wazazi wao.

"licha ya kuwa hatujachukua hatua zozote za kisheria dhidi ya wale wanaohusika na vitendo hivyo, haimaanishi kuwa ni sawa kwa vitendo hivyo kuendelea,'' alisema waziri Soubry