Shambulizi la kigaidi mjini London

Image caption Shambulizi la kigaidi mjini London

Mtu mmoja ameuwawa katika shambulio la mapanga na washukiwa wawili wamepigwa risasi na polisi katika mtaa wa Woolwich, kusini mashariki ya London.

Waziri Mkuu David Cameron amesema kuna ishara nzito kua ni tukio la kigaidi na Uingereza haitaterereka wakati inakabiliwa na mashambulio kama hayo.

Picha za video zimejitokeza zikimuonyesha mtu akipunga panga la kuchinja nyama na kutoa matamshi ya kisiasa.

Akisema " Lazima tupigane nao kama wanavyopigana nasi. Jicho kwa jicho,jino kwa jino".

Taarifa zizisothibitishwa zaeleza mtu aliyeuwawa alikuwa mwanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Woolwich.

Makao ya waziri mkuu yamesema Bwana Cameron ambae alipanga kulala mjini Paris baada ya kukutana na Rais wa Ufaransa anarejea Uingereza.

Waziri wa mambo ya ndani Theresa May aliita mkutano wa kamati ya dharura ya usalama , Cobra.

Watu wote wawili waliopigwa risasi na polisi walipelekwa hospitali na mmoja anasemekana kua katika hali mbaya.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema watu hao wawili walimshambulia mtu mmoja mwenye umri wa miaka 20 ambae alikua amevalia fulana iliyokua na maandishi ya wakfu wa kuwasaidia wanajeshi uitwao Help for Heroes.Msaada kwa mashujaa