Atuzwa kwa kupinga ukeketaji Ethiopia

Image caption Gebre ametuzwa kwa kulaani ukeketaji

Mwanaharakati wa Ethiopia Bogaletch Gebre, ameshinda tuzo ya kimataifa, kwa kampeini yake ya kupambana dhidi ya ukeketaji au tohara kwa wasichana na wanawake.

Bi Gebre alituzwa tuzo yaMfalme Baudouin nchini Ubelgiji kwa kuhamasisha dhidi ya tamaduni au mila ambazo ni haramu kuzungumziwa , kulingana na kamati iliyomteua kuwa mshindi.

Alisaidia katika kupunguza visa vya ukeketaji kutoka 100% ya watoto wasichana hadi kufika 3% katika baadhi ya maeneo ya Ethiopia.

Ukeketaji hufanywa zaidi katika jamii za kiafrika na Mashariki ya kati.

Pia inajulikana kama tohara kwa wasichana ambacho ni kitendo cha kitamaduni kinachiaminiwa kuwafanya wasichana kuendelea kuwa bikira na kisha kumwezesha mwanamke kuoleka.

Katika ukeketejaji sehemu ya siri ya mwanamke hukatwa hali inayomweka mwanamke au msichana yule katika hatari ya kupata magonjwa na hata kupata matatizo wakati wa kujifungua.

Bi Bogaletch aliambia BBC kuwa ujumbe wake kwa viongozi wa kijamii wanaopigia debe ukeketaji, alikuwa na kauli mbiu hii kwao'' Baba wewe uliishi wakati wako, huu ni wakati wetu, wakati wa watoto wetu. Hatutaki kuwaua watoto wetu. Natumai una busara ya kutosha kukubali hilo.''

Wakfu wa Mfalme Baudouin ulimpa Bi Gebre dola 580,000 kama tuzo yake kwa kampeini yake ya kipekee kuhamasisha jamii kuondokana na ukeketaji.

Shirika analofanyia kazi Bi Gebre alisema lilianza kufanya mikutano na wanawake katika maeneo ambayo viwango vya elimu ni vya chini mno na ambako ukeketaji ulikuwa unafanywa kwa sana.

Kwa kutumia kauli mbinu hii kote nchini Ethiopia, ilipeleekea kupunguza visa vya ukeketaji.

Bi Bogaletch aliambia BBC kuwa wanaounga mkono ukeketaji, wanaamini kuwa wanawake wanapswa kudhalilishwa.

"haina uhusiano na utamaduni , hatujui hata jambo hili lilitoka wapi,'' alisema Gebre

"vipi kitu ambacho kinawaua wanawake , kuwadhuru wanawake na watoto kukubalika?''

Mwezi Februari, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa wasichana wachache barani Afrika na Mashariki ya kati, wanakeketwa kwa lazima .

Nchini Kenya visa vya ukeketaji miongoni mwa watoto wadogo vinaendelea kupunguka.