Taharuki mpakani mwa Israel na Lebanon

Image caption Magari ya jeshi la Israel

Wanajeshi wa Israel wanafanya msako katika mpaka wake wa Kaskazini kufuatia ripoti za mashambulizi ya roketi zinazorushwa kutoka Kusini mwa Lebanon

Shirika la habari la Lebanon limesema kuwa makombora ya roketi yamerushwa nchini Israeli kutoka kusini mwa Lebanon. Haijafahamika wazi ni nani aliyefyatua makombora hayo na ni wapi yaliangukia . Jeshi la Israel linasema linachunguza taarifa hizo .

Tukio hilo limetokea wakati hali ya wasi wasi ikitanda katika kanda hiyo kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Syria .

Televisheni ya kundi la Hezbollah ya al-Manar imesema roketi ilirushwa ndani ya Israil usiku wa kuamia leo na kulenga mji wa kusini wa Israil unaojulikana kama Metulla.

Wakaazi wa mji huo wanasema walisikia mlipuko lakini hakuna ripoti kuhusu watu kujeruhiwa au kuuawa.

Televisheni hiyo inasema kikosi cha ulinzi cha Israil kilipelekwa katika eneo la mpakani na hadi sasa hakujatokea mashambulio yoyote. Bado haijulikani ni nani alirusha roketi hiyo.

Wachambuzi wa maswala ya usalama wanasema kuna uwezekano kuwa kundi la Hezbollah halikuhusika na huenda waliotekeleza shambulio hilo walitaka kuchochea mzozo kati ya Israil na kundi hilo.