Je vikwazo vya silaha dhidi ya Syria vilegezwe?

Image caption Uingereza na Ufaransa zitaka kutuma silaha kwa wapinzani wa Assad Syria

Mawaziri wa mambo nje wa Muungano wa Ulaya , wanajadili hoja iliyotolewa na Ufaransa na Uingereza ya kulegeza vikwazo vya silaha dhidi ya Syria ili wapiganaji waweze kupokea silaha kutoka kwa nchi hizo mbili.

Ufaransa na Uingereza zinatarajiwa kutetea hoja hiyo wakisema hatua hiyo itaweza kuongeza shinikizo kwa serikali ya Syria kutafuta mwafaka wa kisiasa.

Uingereza na Ufaransa zinataka vikwazo kulegezwa ili waweze kutuma silaha kwa ule wanaoutaja kuwa ni upinzani wa kadri nchini Syria.

Mkuu wa kitengo cha udhibiti wa silaha katika shirika la Oxfam, Anna McDonald, amesema kuwa kutuma silaha kwa upinzani nchini Syria kutachochea kusambaa zaidi kwa silaha nchini humo.

Hata hivyo, nchi za Muungano wa Ulaya, zinapinga kuondolewa kwa marufuku ya kuingiza silaha nchini humo ambayo inakamilika Mei tarehe 31.

Maafisa wa Ulaya wameonya dhidi ya kuhatarisha mpango wa sasa wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa amani.

Ikiwa hapatakuwa na makubaliano kuhusu kuongeza muda wa marufuku hiyo au la, vikwazo vingine vya kuongeza shinikizo dhidi ya serikali ya Assad pamoja na washirika wake, huenda pia ikaisha. Hilo ndilo jambo wanalotaka kuzuia maafisa wakuu wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria, amethibitisha kuwa serikali itahudhuria mkutano huo wa amani ambao Marekani na Urusi zinatumai utafanyika mjini Geneva mwezi Juni.

Walid Muallem alisema kuwa itakuwa fursa nzuri kwa kutafuta mwafaka kwa mzozo huo ambao Umoja wa mataifa unasema umesababisha vifo vya zaidi ya watu 80,000.

Wanachama wa upinzani wanajadili ikiwa watahudhuria mkutano huo , lakini msemaji wao ameelezea kuwa wataweza kufika kwenye mkutano huo ikiwa rais Bashar al-Assad atakubali kuondoka mamlakani.