Mkuu wa baraza la Congress ajiuzulu Libya

Image caption Muhammad al-Magarief

Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la Congress nchini Libya amejiuzulu kufuatia kupitishwa kwa sheria mpya inayoharamisha yeyote aliyefanya kazi katika serikali ya hayati Muamar Gaddafi kushikilia wadhifa wowote katika serikali ya sasa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari,Muhammad al-Magarief alisema kuwa bunge ilipitisha sheria inayowatenga watu waliofanya kazi katika serikali ya Gaddafi, na kuwa kila mtu anapaswa kuitii sheria hiyo.

Aidha sheria hiyo, imekosolewa sana kwa kuwa na nguvu sana.

Kanali Gaddafi aliondolewa mamlakani mwezi Agosti mwaka 2011.

"najiuzulu na ninafanya hivyo kwa roho safi nikiwa najivunia kwa kufanya hivyo," alisema bwana Magarief, alipokamilisha hotuba yake ya dakika 40, kwa baraza la Congress.

Hata hivyo haijulikani kwa sasa ikiwa wanachama wa Congress, wanahitajika kupiga kura kuhusu ikiwa watalikubali au kulikataa ombi la bwana al-Magarief kujiuzulu.

Hata hivyo, kufuatia taarifa yake, msemaji wa Congress, Omar Hmeidan, alisema kuwa baraza la Congress litahitajika kumteua mwenyekiti mwengine .

Chini ya sheria mpya, mabalozi waliofanya kazi chini ya utawala wa Gaddafi hawawezi kuendelea kushikilia nyadhifa zao.

Kulikuwa na mjadala mkali kuhusu mabadiliko yanayofanyiwa sheria hiyo, kuruhusu baadhi ya maafisa kushikilia nyadhifa hiyo , lakini hilo bado halijafanyika.

Dr Magarief alihudumu kama balozi nchini India, kwa miaka miwili, katika miaka ya themanini kabla ya kuondoka katika serikali ya Gaddafi.

Aliishi uhamishoni kwa miaka 31 kama kiongozi wa vuguvugu la ukombozi wa Libya.