Wapiganaji tisho kwa Afrika Magharibi

Image caption Rais John Mahama anaona kama wapiganaji wa kiisilamu ni tisho kwa Afrika Magharibi

Rais wa Ghana, John Mahama, ameonya kwamba wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu wanazusha tishio linaloweza kuvuruga amani katika eneo zima la Afrika magharibi.

Licha ya kwamba Ghana haijaathirika moja kwa moja, rais Mahama amesema hakuna nchi ilio salama iwapo wanamgambo hao wataruhusiwa kudhibiti eneo jingine.

Katika mahojiano na BBC Rais wa Ghana John Dramani Mahama amesema kuwa wakati umewadia bara la Afrika Kubuni kikosi maalum cha kupambana na ugaidi-akipendekeza kikosi hicho kifadhiliwe na kodi inayotozwa safari za ndege na huduma za mikahawa kote barani Afrika.

Amesema mataifa ya Afrika yanahitaji kushirikiana kwa pamoja katika ulinzi na kudumisha amani huku akiongeza kuwa hakuna taifa ambalo litakuwa salama ikiwa maasi yataruhusiwa kutekelezwa kwingineko.

Mwezi Januari , majeshi ya Ufaransa yaliongoza operesheni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu na wapiganaji wengine kutoka Kaskazini mwa Mali ambako waliteka sehemu kubwa ya eneo hilo baada ya mapinduzi ya kijeshi kumng'oa mamlakani aliyekuwa rais wa Mali mwaka jana.

Rais Mahama alisema tukio hilo lilionyesha kuwa eneo zima la Sahel, limekuwa kivutio kikubwa kwa makundi ya kigaidi .

"ikiwa hatutakabiliana na wapiganaji hao, eneo hili litakosa uthabiti,'' rais Mahama aliambia BBC.

Licha ya kutwaa uthabiti kutoka kwa makundi ya wapiganaji wa Mali, mzozo wa Mali ungali tisho kubwa la usalama.

''Kuna tisho la mashambulizi kama yale tuliyoyaona nchini Niger, kwa siku za mwisho tulizoziona, kwa hivyo ni jambo ambalo bado linaleta wasiwasi katika eneo hilo,'' alisema Mahama