Washukiwa wa Woolwich mahakamani London

Mshukiwa wa mauaji ya mwanajeshi nchini Uingereza hii leo alifikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji ya Lee Rigby katika mtaa wa Woolwich,Kusini mashariki mwa London.

Michael Adebowale, mwenye umri wa miaka 22, aliyekuwa na pingu mikononi , aliongea tu kuthibitisha kuwa ndiye mshukiwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake katika mahakama ya Westminster.

Michael Adebowale alitoka hospitalini baada ya kutibiwa kwa jeraha la risasi aliyipigwa na polisi.

Alijerejeshwa rumande huku akitarajiwa kufika mahakamani Jumatatu wiki ijayo.

Bwana Adebowale alifikishwa mahakamani baada ya kulazwa hospitalini kwa siku sita kufuatia jeraha alilopata baada ya kupigwa risasi na polisi siku aliyomshambulia mwanajeshi na kumuua.

Mshukiwa wa pili angali anazuiliwa na polisi.

Bwana Michael Adebolajo, 28, anayeendelea kupokea matibabu hospitalini pia alipigwa risasi na polisi wakati alipokamatwa.

Siku ya Jumatano, uchunguzi wa madaktari ulibaini kuwa mwanajeshi Drummer Rigby, aliyekuwa na umri wa miaka 25, alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kisu katika barabara moja ya mtaa wa Woolwich, karibu na kambi za jeshi

Ulinzi mkali

Bwana Adebowale, ambaye pia ameshtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha, alifikishwa mahakamani akiwa na bendeji mkononi huku akiwa amezingirwa na maafisa wa polisi.

Alionekana kuchechemaa alipokaribia kuingia mahakamani.

Washukiwa hao wawili, Adebowale na Adebolaj, walinaswa kwa video na kupigwa picha na waliowashuhudia wakifanya shambulizi lao nyakati za mchana.