Vijana wa Malawi waenda Korea kwa ajira

Image caption Rais Joyce Banda anasema Malawi inakabiliwa na wakti mgumu kuhusu ajira kwa vijana

Serikali ya Malawi, imetetea mpango wake tatanishi ulioafikiwa na Korea Kusini kusafirisha hadi vijana wake laki moja kufanya kazi kama wafanyakazi wahamiaji.

Wabunge wa upinzani wametaja mpango huo kama biashara ya utumwa.

Lakini waziri wa wafanyakzi nchini humo anayekabiliwa na wakati mgumu kuwatafutia ajira vijana amekanusha madai hayo.

Eunice Makangala, aliambia BBC kuwa alitaka tu kusaidia vijana wa Malawi wanaotarajiwa kwenda Seoul kutafutiwa ajira.

Mwandishi wa BBC mjini Blantyre anasema, Rais Joyce Banda, aliweka mkataba huo na serikali ya Korea Kusini wakati alipozuru nchi hiyo mwezi Februari, mwaka huu.

Makubaliano hayo yatashuhudia vijana wenye kati ya umri wa miaka 18-25 kupata kazi katika viwanda vya nchi hiyo na hata kwenye mashamba katika rasi ya Korea.

Hakuna takwimu rasmi za viwango vya ukosefu wa ajira nchini Malawi, kwa sababu ya kutokuwepo mfumo wa kutambulisha watu, kuweza kujua idadi ya wasio na ajira.

Lakini utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa 80% ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu hurejea vijijini kila mwaka kwani hawezi kupata kazi mijini.

Lakini wabunge wa upinzani wameghadhabishwa mno kwa sababu ya mpango wa kutaka kuwasfirisha vijana hao kutafuta kazi nchini Korea.

''Daima sisi hulalamika kuhusu wataalamu wetu kwenda kutafuta ajira katika nchi za kigeni, na hata kuwashawishi raia wa Malawi wanaoishi katika nchi za kigeni kurejea nyumbani, wakati hapa tunawapeleka vijana kutafuta ajira nje? alilalamika mbunge mmoja.

Bi Makangala aliambia BBC kuwa wameafikia mpango huu kwa nia njema.

''Sio utumwa mambo leo'', alisisitiza bi Makangala

''Kuna watu wanaofanya hapa kazi na ambao wanatoka Misri, Nigeria, India na Uingereza.''

"je unataka kuniambia watu hao ni watumwa? Na viwango vya ukosefu wa ajira viko juu sana .''

Lakini Henry Kachaje,ambaye ni mtaalamu wa maswala ya ajira alisema kuwa mktaba ungeweza kuafikiwa vyema kuliko makubaliano ya sasa. Kuwa serikali ingwavutia wakeezaji kuja nchini humo na kutoa nafasi ya ajira kwa vijana.