Dola milioni 7 kwa mwenye habari kuhusu Boko Haram

Image caption Kiongozi wa wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram, Abubakar Shekau

Marekani inaahidi kutoa zawadi ya fedha kwa yeyote atakayetoa habari kuhusu makundi ya wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini na Magharibi mwa Afrika.

Wizara ya mambo ya ndani nchini Marekani inasema itatoa dola milioni saba kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu aliko kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau.

Zawadi nyingine za kima kidogo pia zitatolewa kwa wale watakaokuwa na habari kuhusu viongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Kaskazini mwa Afrika na wale wa kundi la (Movement for Unity and Jihad) Afrika Magharibi.

Yeyote atakayepasha habari kuhusu kiongozi wa zamani wa kigaidi Mokhtar Belmokhtar ataweza kupokea dola milioni tano.

Kundi lake la wapiganaji lijulikanalo kama, Blood Battalion,linasemekana lilifanya shambulizi dhidi ya kiwanda cha gesi, Kusini mashariki mwa Algeria mwezi Januari ambapo mateka 37 waliuawa wakiwemo wamarekani watatu.

Donge nono la dola milioni tano pia lilitolewa kwa mtu ambaye angetoa habari kumhusu kamanda mkuu wa wapiganaji wa kiisilamu Yahya Abu el Hammam, ambaye Marekani ilipanga kushambulia watu na kuwateka nyara wageni katika kanda ya Afrika Magharibi.

Wizara hiyo ilisema kuwa takriban dola milioni 3 zitatolewa kwa watakaotoa habari kuhusu viongozi wengine wa kigaidi wakiwemo, Malik Abou Abdelkarim na msemaji wa kundi la (Mujao) Oumar Ould Hamaha.

Inaarifiwa kuwa Oumar Ould Hamaha, alihusika na visa vya utekaji nyara wa raia wa kigeni nchini Niger mwaka 2008 na kudai kulipwa kabla ya kuwaachilia

Kundi la Boko Haram, limekuwa likifanya mashambulizi makali Kaskazini mwa Nigeria, na kusababisha vifo vya watu 2,000 tangu mwaka 2009.

Kumekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuwepo uhusiano kati ya Boko Haramna makundi mengine ya kigaidi katika nchi zingine katika kanda hiyo ikiwemo kundi la AQIM.