Akina mama kujifungua bure Kenya. Inawezekana?

Serikali nchini Kenya imeanza kutekeleza ahadi yake ya kufutilia mbali malipo yanayotozwa akina mama wajawazito kujifungua katika hospitali za umma kote nchini.

Rais Uhuru Kenyatta aliahidi katika manifesto yake ikiwa atachaguliwa kama rais kufutilia mbali ada inayotozwa na hospitali za umma kwa akina mama kujifungua katika siku miamoja za kwanza za uongozi wake.

Kufikia hapo jana , moja ya hospitali kubwa za huduma kwa wanawake, ya Pumwani, iliwaruhusu wanawake zaidi ya tisini waliojifungua kurejea nyumbani bila kutozwa chochote.

Mpango huu unatekelezwa kote nchini, katika hospitali, zahanati na hata katika kliniki za umma.

Gavana wa jimbo la Nairobi, Evans Kidero alisisitiza kuwa ada inayotozwa wanawake tangu wanapolazwa hospitalini hadi wanapojifungua, itagharamiwa katika mpango huu wa serikali kwa kiwango cha shilingi bilioni 8.

Image caption Hospitali ya Pumwani inasemekana kuhitaji zaidi ya shilingi bilioni mbili kukarabatiwa

"Akina mama wote waliojifungua katika hospitali ya Pumwani wanaruhusiwa kwenda nyumbani bila malipo kuambatana na agizo la rais Kenyatta. Pumwani ni moja ya hospitali kubwa ya wanawake kusini mwa jangwa la Sahara,'' alisema gavana Evans kidero.

Rais Kenyatta alifutilia mbali ada wanayotozwa wanawake wanapojifungua katika taasisi za serikali katika kile alichotaka kuwa sehemu ya juhudi za serikali ya Jubilee kutekeleza malengo yake

Kwa upande wake waziri wa afya James Macharia, alisisitiza kuwa hakuna hospitali yoyote ya umma inapaswa kutoza ada yoyote.

"Yeyote aliyelipishwa kwa huduma walizopata, anapaswa kurejeshewa pesa zake. ''

''Ruwaza ya Jubilee, ilithibitisha kuwa tunaweza kutoa huduma za bure kwa akina mama na huu ndi mwanzo wa safari yetu (mpango huu).'' alisema waziri Macharia

Aidha alisisitiza kuwa malipo kwa huduma yoyote yataweza kugharamiwa na serikali.

Katika vituo vya afya vya umma mashinani, mwanamke huhitajika kulipa shilingi 2,500 au dola 31 ,katika baadhi ya vituo kote nchini, baadhi hutozwa shilingi 5,000 au dola sitini na mbili wakati katika hospitali kuu ya serikali, akina mama hutozwa dola zaidi ya miambili.

Image caption Wanawake wanatabasamu kwa kuweza kujifungua bila malipo

Gharama hizo zote zitakuwa jukumu la aserikali sasa haijalishi matatizo watakayokabiliwa nayo wanawake, yote yatagharamiwa.

Bwana Macharia, alisema kuwa katika siku miamoja zijazo wizara ya afya itatumia shilingi bilioni moja kutoa huduma za afya ya uzazi kwa akina mama na kisha kuanzia mwaka ujao, inatumia bilioni nane kila mwaka kuwezesha akina mama kupokea huduma hizo.

Tayari mpango huo umeshajadiliwa na hazina ya serikali na wizara imepewa kipaombele katika kuhakikisha kuwa inapokea pesa hizo.

Amewataka wananchi kutumia fursa hiyo ili kupunguza idadi ya vifo vya akina mama na watoto wachanga.

Hata hivyo licha ya kuwa hii ni habari njema kwa wanawake, bado kuna changamyo si haba. Tayari siku moja tu tangu kuanza kwa mpango huo, mwanamke mmoje mkoani Pwani amepoteza mwanawe kwa kile wanachokiita kupuuzwa na wauguzi wakati mama huyo alikaribia kujifungua.

Mtoto wa mama huyo kwa jina Margaret Munavu, alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa na sasa wanalaumu wauguzi kwa kutokuwa maakini. Mama huyo alijifungulia katika hospitali kuu ya serikali katika jimbo la Mombasa.

Changamoto zengine zinazokabili sekta ya afya nchini Kenya ni pamoja na ukosefu wa vifaa , akina mama kulazimika kuja hospitalini na nyembe,pamba, na vifaa vingione vinavyohitajika wanapojifungua.

Baadhi ya hospitali na vituo vingine ziko katika hali mbaya kiasi cha kuhitaji ukarabati. Katika hospitali ya Pumwani , mjini Nairobi, ambayo ndiyo kubwa zaidi katika kuwahudumia akina mama wajawaziti Kusini mwa jangwa la Sahara, huwashughulikia takriban wanawake miamoja au zaidi kwa kujifungua pekee.

Wakosoaji wanasema ni bora kwa serikali mwanzo kukarabati nyingi ya hospitali za umma kabla ya kuanza kutoa huduma ya bure ya uzazi kwa wanawake.