Sudan yazuia misaada kwa watu 120,000

Image caption Watu waliokimbia makwao nchini Sudan

Shirika moja la kutoa misaada ya kibinadam nchini Sudan, limedai kuwa serikali ya nchi hiyo inazuia usambazaji wa misaada ya kibinadam kwa zaidi ya watu laki moja wanaoishi katika maeneo tepetepe.

Shirika hilo limesema watu hao walikimbia makwao kutokana na mapigano yanayoendelea katika jimbo la Jonglei kati ya jeshi la serikali na waasi.

Shirika hilo la Medecins Sans Frontieres (MSF), limesema kuwa watu hao kwa sasa hawana maji safi ya kunywa, chakula au dawa na hivyo kukabiliwa na tishio kubwa na kuangamia.

Aidha limesema kuwa eneo hilo lina mbu wengi na hivyo kutishia mlipuko wa ugonjwa wa Malaria.

Serikali ya Sudan Kusini imesema kuwa utawala wa Khartoum unatoa msaada wa kijeshi kwa makundi ya wapiganaji wa waasi wanaoendesha harakati zao katika eneo hilo, madai ambayo yamekanushwa vikali na serikali ya Sudan.

Kwa upande wake serikali ya Sudan imedai kuwa serikali ya Sudan Kusini ndio inayotoa msaada kwa makundi ya waasi yanayopinga utawala wake.

Jimbo la Jonglei limekumbwa na mapigano ya kikabila tangu eneo la Sudan Kusini kujitangazia uhuru wake kutoka Sudan Julai mwaka wa 2011.

Eneo la Pibor ndilo lililoathirika zaidi.