Askari wa kikosi maalum wauawa Libya

Wandamanaji mjini Benghaz
Image caption Wandamanaji mjini Benghaz

Askari 6 wa kikosi maalum wameuawa usiku wa kuamkia leo na watu mwenye silaha waliojifunika nyuso Mashariki mwa mji wa Benghazi nchini Libya.

Mkuu wa jeshi mjini humo ameiambia BBC, kwamba watu hao wenye silaha wameshambulia makao makuu ya kikosi maalum cha kijeshi.

Afisa huyo aliongeza kusema mapigano makali yalitokea kati ya wanajeshi wake na wanamgambo hao.

Benghazi ilikuwa kitovu cha uasi uliong'oa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Mji huo haukutulia na umekumbwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wanamgambo waliokuwa waasi na jeshi la serikali sasa.

Mapigano ya kikabila

Wanamgambo kutoka koo mbali mbali na wenye itikadi kali wanadhibiti baadhi ya sehemu za mji huo ulioshuhudia wimbi la mashambulio dhidi ya jeshi la serikali.

Image caption Wapiganaji wa waasi nchini Libya

Katika mtandao wa kijamii wa Facebook wa kikosi hicho maalum cha jeshi picha za kutisha za baadhi ya askari walioawa mapema jumamosi asubuhi zimechapishwa.

Mwandishi wa BBC Rana Jawad, amesema wawili miongoni mwa waliouawa wameonekana kuuawa baada ya kutekwa nyara na watu ambao kikosi hicho maalum kimeeleza kuwa ni wapiganaji wa kundi la Takfir cha Waislam wenye itikadi kali.

Mapigano ya hivi karibuni ni ishara ya mwendelezo wa mashambulio dhidi ya kikosi maalum tangu kilipopelekwa katika mji huo mwezi mmoja uliopita.

Matukio ya awali yalikuwa ni pamoja na kuvishambulia vituo vya ukaguzi vya barabarani.

Makundi ya Kiislam yenye itikadi kali yalishutumiwa kuhusika na shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, mwezi Septemba mwaka uliopita ambapo raia 4 wa Marekani waliuawa akiwemo balozi Chris Stevens.