Amisom yalaani shambulio Somalia

Image caption Wapiganaji Somalia

AMISOM yashutumu shambulio katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu

Mjumbe maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (SRCC) nchini Somalia, Balozi Mahamat Saleh Annadif ameshutumu vikali shambulio la kigaidi lililofanywa leo na magaidi wa Al-Shabaab katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu.

"Tunalaani vikali shambulio hili la kinyama katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu. Mashambulio haya yasiyofanikiwa yanayoendeshwa na Al-Shabaab yanalenga tu kuvuruga jitihada zinazochukuliwa na wananchi wa Somalia baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya ishirini na magaidi hao hawawezi kuzuia jitihada zetu za pamoja kuendelea kuwasaidia wananchi wa Somalia kuijenga nchi yao" amesema Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (SRCC), Balozi Mahamat Saleh Annadif.

Balozi Mahamet Annadif amepongeza hatua ya haraka iliyochukuliwa na majeshi maalum ya AMISOM na majeshi ya usalama ya Somalia na amesisitiza kuwa AMISOM haitaacha kuchukua hatua za kuimarisha usalama nchini Somalia.

"Umoja wa Afrika na AMISOM kwa sasa wako pamoja na wananchi wa Somalia," amesema Balozi Annadif, wakati akituma salaam za rambirambi kwa wale waliowapoteza wapendwa wao katika shambulio hilo na kuwaombea kupona haraka watu wote waliojeruhiwa.