15 wauawa kwenye mashambulizi Kenya

Image caption Mji wa Mandera umekuwa kitovu cha mashambulizi ya maguruneti katika mpaka wa Kenya na Somalia na sasa mamia wameanza kuukimbia

Watu 15 wameuawa katika mashambulizi ya gurunrti Kaskazini mashariki mwa Kenya , karibu na mipaka ya Somalia na Ethiopia.

Zaidi ya wengine 20 walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Banisa mjini Mandera.

Ghasia ziliripotiwa kuzuka katika kambi ya watu waliopoteza makao yao.

Yanakuja baada ya makabiliano mengine siku ya Ijumaa kati ya koo mbili katika eneo hilo ambapo watu sita waliuawa.

Mamia ya watu wanasemekana kutoroka eneo hilo.

Polisi wameweza kudhibiti hali.

Afisaa mmoja wa polisi mjini Mandera, alinukuliwa akisema kuwa miongoni mwa waliouawa alikuwa mkimbizi mmoja wa ndani akiwa mmoja wa wale waliopoteza makao yao kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Hadi sasa hakuna kundi lolote limekiri kufanya mashambulizi hayo.

Kiongozi wa kijamii Ibrahim Hussein, ambaye amekuwa akihusika na juhudi za kusitisha ghasia, kati ya koo za Degodia na Gari kuwataka kusalimisha silaha anasema hali ingali tete.

Duru zinasema kuwa wale wanaoamika kufanya mashambulizi hayo ni watu kutoka nchini Ethiopia na walikuwa wanalenga gari lililokuwa limembeba kamishna mkuu wa mji wa Banisa.

Kwingineko Viongozi wa Kaunti ya Mandera, wametakiwa kufika katika ofisi za idara ya ujasusi kuandikisha taarifa kuhusu makabiliano yanayoendelea huko kati ya koo hasimu.

Mkuu wa polisi David Kimaiyo aliwataka viongozi hao kufika kutoa taarifa zozote walizonazo kuhusu mapigano ya kiukoo yaliyokuwa yanaendelea huko. Zaidi ya watu ishirini waliuawa kuanzia Ijumaa katika mapigano hayo yaliyoathiri Mandera na kaunti jirani ya Wajir.

Mapigano yanayoshuhudiwa yemaingia katika mwezi wake wa tatu tangu yaanze na hata kuenea kutoka Mandera hadi Wajir.