Kero la uharamia Afrika Magharibi

Image caption Uharamia umekita mizizi katika Ghuba ya Guinnea

Viongozi wa kanda ya Afrika Magharibi, wametoa wito wa kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha jeshi la wanamaji kukabiliana na tishio la uharamia katika ghuba ya Guinea.

Uharamia katika eneo hilo unahitaji kukabiliwa kwa ''mkono mkali wa kisheria ,'' alisema rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara kwenye mkutano wa viongozi wa kikanda.

Wakati huu kuna mashambulizi zaidi yanayofanywa na maharamia katika ghuba ya kanda ya Afrika Magharibi kuliko kwenye fuo za Somalia. Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la mabaharia.

Ushikaji doria unaofanywa na wanajeshi wa kimataifa umepunguza visa vya uharamia.

Takriban mabaharia 960, walishambuliwa Afrika Magharibi mwaka 2012 pekee ikilinganishwa na 851 waliokamatwa katika pwani ya Somalia.

Hii ni mara ya kwanza kwa visa zaidi vya mashambulizi yanayofanywa na maharamia kuripotiwa katika fuo za Guinea kuliko hapo awali.

Eneo linalokabiliwa na tisho zaidi ambako uharamia unatendwa Afrika Magharibi ni katika pwani ya Nigeria, nchi inayozalisha viwango vikubwa zaidi vya mafuta ghafi barani Afrika .

Akihutubia mkutano wa viongozi wa Afrika Magharibi na Kati, mjini Yaounde, bwana Ouattara alitoa kauli hii,: "naitaka jamii ya kimataifa, kuweka sheria kudhibiti uharamia katika Ghuba ya Guinea kama walivyokuwa wakali kuhusu uharamia katika pwani ya Somalia, ambako uwepo wa wanajeshi wa kimataifa kumesaidia katika kupunguza visa vya uharamia.''

Naye rais wa Cameroon,Paul Biya, alisema kuwa ni muhimu kuchukua hatua kulinda, meli na mabaharia pamoja na maslahi ya kiuchumi katika kanda hiyo.

Maharamia katika kanda ya Afrika Magharibi, zaidi huiba mafuta pamoja na mali za wasafiri huku wakitumia mabavu kufanya vitendo vyao.

Watano kati ya mahabaria 206 waliotekwa nyara mwaka jana , waliuawa katika ghuba ya Guinea.

Hata hivyo ikilinganishwa na ambavyo maharamia wa kisomali huendesha shughuli zao, wao huwazuilia maharamia hadi wanapolipwa kikombozi ndio wanawaachilia.