S. Kusini kupata suluhu zogo la mafuta

Image caption Ramani ya Sudan Kusini

Sudan Kusini imepiga hatua kubwa katika azma yake ya kutaka kuuza mafuta katika mataifa yaliyo eneo la kusini.

Marais wa Uganda, Kenya na Rwanda wamekubaliana kujenga mifumo miwili ya mabomba ya kusafirisha mafuta katika eneo la Afrika Mashariki.

Mojawepo wa mifumo hiyo itatokea nchini Sudan Kusini hadi katika mji wa bandari wa Lamu nchini Kenya huku mfumo wa pili ukijengwa kutoka Rwanda hadi mjini Mombasa.

Kwa sasa Sudan Kusini inauza mafuta yake kupitia Jamhuri ya Sudan lakini mauzo hayo huvurugwa mara kwa mara kutokana na tofauti zinazozuka kuhusiana na bei pamoja na mswala ya kiusalama.

Makubaliano hayo yanayoshirikisha mataifa matatu yamethibirishwa na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uganda, Sam Kutesa.

Wiki iliyopita rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir alitishia kusitisha tena usafirishaji wa mafuta kutoka Sudan Kusini kupitia mipaka ya taifa lake, ikiwa Sudan Kusini haitakoma kuwaunga mkono waasi wanaondeleza harakati zao katika eneo la mpakani baina ya nchi hizo mbili.

Sudan Kusini inakanusha kuwaunga mkono waasi hao, na badala yake inaishutumu Khartoum kwa kuchochea maasi Sudan Kusini.

Wakati Sudan Kusini iliponyakuwa uhuru yapata miaka miwili iliyopita, iliondoa asilimia 75 ya visima vya mafuta kutoka Sudan.

Hata hivyo, Sudan ilisalia na mfumo wa mabomba ya kusafirisha mafuta hayo viwanda vya kuyasafisha pamoja na bandari ya Port Sudan kwenye bahari nyekundu.

Eneo la Afrika mashariki linashuhudia kwa sasa maendeleo makubwa katika sekta ya kawi baada ya mafuta na gesi kugunduliwa nchini Kenya, Uganda na Tanzania.

Mfumo mpya wa reli.

Kadhalika waziri Kutesa amesema kuwa mataifa hayo matatu yamekubaliana kujenga mfumo mpya wa reli kutoka Kenya, kuelekea Uganda hadi Rwanda.

''Makubaliano yaliyopo ni kwamba mfumo wa reli uliopo ufanyiwe ukarabati pamoja na kujenga mfumo wa kisasa wa reli kutoka Kenya hadi Uganda na kisha Rwanda,'' amesema bwana Kutesa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii