Uingereza kupiga marufuku Miraa

Image caption Mmea wa Miraa

Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa mmea wa Miraa au Mirungi utapigwa marufuku.

Mmea huo ambao hutafunwa ni maarufu miongoni mwa watu wenye asili Kisomali, Yemen na Ethiopia nchini Uingereza.

Hata hivyo uamuzi huo uliotolewa na waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, Teresa May, unaenda kinyume na mapendekezo yaliyotolewa na washauri wa serikali wa masuala ya tiba, ambao mwezi Januari mwaka huu walipendekeza mmea huo uendelee kuwa halali.

Ikiwa sheria hiyo itaidhinishwa, miraa itakuwa miongoni mwa dawa za kulevya za daraja C zilizoharamishwa na wale watakaopatikana na hatia ya kuuza au ktumuia miraa au mirungi watahukumiwa kifungo cha hadi miaka kumi na minne gerezani na faini kubwa.

Jopo la wataalamu lilisema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mmea huo unasababisha matatizo ya kiafya au uhalifu.

Lakini May amesema uraibu wa utafunaji wa Miraa umekuwa na athari kubwa nchini Uingereza.Tayari serikali ya Uingereza imelijulisha bunge kuwa itawasilisha muswada bungeni ili kuidhinisha pendekezo hilo kuwa sheria.

Image caption Mteja wa Miraa akizitafuna

Tangazo hili halijapokelewa vizuri na wafanyabiashara wa miraa, ambapo wamelalamika kuwa serikali inataka kuwapokonya biashara yao na kusababisha ukosefu wa kazi.

Wakulima wa miraa nchini Kenya pia wataathirika kwa kukosa soko barani ulaya.

Katika miezi ya hivi karibuni, shehena za miraa zilizokuwa zikisafirishwa kuelekea nchini Uholanzi kutoka Uingereza zimenaswa na maafisa wa idara ya uhamiaji baada ya serikali ya nchi hiyo kupiga marufuku uuzaji na utafunaji wa miraa mwaka uliopita.

Miraa imepigwa marufuku katika mataifa mengi ya muungano wa ulaya pamoja na Canada na Marekani.