Muda wayoyoma kwa rais Morsi wa Misri

Rais wa Misri Mohammed Morsi

Hali ya taharuki imetanda Misri huku makataa iliyotolewa na jeshi kwa rais wa nchi hiyo Mohammed Mosri ikikaribia kufika ukingoni.

Kuna taarifa za kutofautiana kuhusu ikiwa jeshi litatoa taarifa punde baada ya muda huo wa masaa 48 aliopewa rais Morsi kutafuta suluhu ya mgogoro huo kutimia.

Jeshi linasemekana tayari kudhibiti jengo la televisheni ya taifa.

Maafisa wakuu wa serikali wako kwenye mkutano wa dharura nchini Misri, saa chache kabla ya muda wa mwisho ambao jeshi na upinzani zilimpa rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo.

Jeshi limesema kuwa litaingilia mzozo unaokumba nchi kwa kutoa mpango wake maalum wa kutatua mgogoro huo, ikiwa pande zote mbili hazitaafikiana.

Wafuasi na wapinzani wa rais Morsi wanaanza kujitokeza barabarani kwa maandamano kwa siku ya nne tangu kuanza mwishoni mwa wiki jana.

Kwa upande wake RaisMohammed Morsi amesisitiza kwamba yeye ndiye kiongozi halali wa taifa huku maandamano kati ya wapinzani na wafuasi wake yakisababisha vifo zaidi.

Kwenye hotuba aliyotoa kwa taifa usiku wa kuamkia leo, Mosri alipinga makataa ya jeshi kutatua mgogoro wa sasa ifikapo Jumanne. Kiongozi huyo amesema hataamrishwa na yeyote na kuwasihi waandamanaji kuweka utulivu.

Hata hivyo watu 16 walikufa katika moja wapo ya maandamano ya wafuasi wa Morsi. Awali jeshi lilitoa mpango wa kurejesha taifa katika uthabiti.

Stakabathi iliyopatikana na BBC inasema jeshi linapanga kuvunja katiba, kuweka machakato wa uchaguzi mkuu, na kuvunja bunge.

Hapo Jumatatu Jeshi lilisema huenda likaingilia kati ikiwa hali haitabadilika. Morsi na wanasiasa walipewa saa 48 kuafikiana.