Tsvangirai alalamikia mageuzi Zimbabwe

Image caption Mugabe analalamika kuwa serikali haijafanya mageuzi ya kutosha

Mageuzi yanayotakikana kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki wa urais , nchini Zimbabwe baadaye mwezi huu, bado hayajafanywa. Hii ni kwa mujibu wa waziri mkuu Morgan Tsvangirai.

Pia aliahidi kubuni nafasi, za kazi alipozindua kampeini yake katika mkutano wa hadhara eneo la Marondera, kabla ya uchaguzi kufanyika Julai tarehe 31.

Anawania urais dhidi ya mpinazni wake mkuu na wa muda mrefu, Robert Mugabe.

Mnamo Ijumaa rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89 alisema uchaguzi huo utakuwa wa kufa kupona lakini akawaahidi wafuasi wake kujizuia na ghasia.

Mugabe alitabiri kupata ushindi wa asilimia 90.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu ghasia na vitisho kabla ya uchaguzi kufanyika.

Ajira, Afya na Uchumi

Bwana Tsvangirai anajitosa kwenye ulingo akiwa shingo upande, kwani mageuzi muhimu kabla ya uchaguzi kufanyika bado hayajatekelezwa.

Aliambia umati wa wafuasi wake kuwa bado mageuzi hayajafanywa katika vyombo vya habari pamoja na mabadliko mengine kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Tsvangirai aliyekuwa anahutubia watu mjini Harare, aliahidi chama chake kitabuni nafasi za kazi na kuimarisha viwanda vinavyozalisha bidhaa pamoja na uzalishaji wa madini ambavyo vimefungwa kwa muda mrefu.

Pia aliahidi kuanzisha huduma bure za afya katika siku za kwanza miamoja za utawala wake ikiwa atashinda uchaguzi. Pia ameahidi kuondoa malipo ya uzazi kwa wanawake hospitalini.

Lakini alisema kuwa atarejesha tu dola ya Zimbabwe ikiwa uchumi wa taifa hilo utaimarika.

Alijiondoa kwenye duru ya pili ya kinyang'anyiro cha urais cha mwaka 2008 akituhumu polisi na kikosi cha usalama cha Mugabe kwa kushambulia wafuasi wake kote nchini.

Alishinda kura nyingi katika duru ya kwanza lakini kulingana na matokeo rasmi hayakutosha kumpa ushindi wa moja kwa moja.

Badaaye Mugabe alishinda duru ya pili kwa asilimia 85% ya kura zilizopigwa huku kiongozi wa kikanda wakiwashauru wawili hao kuwa na serikali ya mseto kugawana madaraka.