Wanaharakati walaani hali Sudan Kusini

Image caption Sudan Kusini ilijipatia uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011

Vugu vugu moja la wamarekani waliosaidia Sudan Kusini kupata uhuru wake miaka miwili iliyopita, wameituhumu serikali kwa kukiuka haki za binadamu pamoja na ufisadi.

Katika ujumbe wake wa barua kwa rais Salva Kiir, wanaharakati hao wanaojiita marafiki wa Sudan Kusini, wamesema kuwa nchi hiyo iko katika hali mbaya.

Wanatuhumu maafisa wa usalama kwa kuwalenga raia kwa sababu za kiukabila na wanasema kuwa serikali imekosa kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi wake.

Wanaharakati hao wakiwemo maafisa wakuu wa zamani katika serikali ya Marekani walisema kwamba hahawezi kupuuza hali nchini humo wakati waathiriwa wa siku za nyuma ndio wamegeuka na kuwa wakiukaji wakuu wa haki za binadamu.

Sudan Kusini, ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011 baada ya miaka mingi ya kuzozana na serikali ya Khartoum.